Serikali ya awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, inaendeleza hatua ya utafiti wa uanzishwaji wa matumizi ya Sarafu za Kidijitali za Benki Kuu.
Akijibu swali la Mbunge wa Jimbo la Kigamboni, Mh. Faustine Ndungulile, aliyeuliza Serikali ina mpango gani wa kuanza kwa matumizi ya Sarafu za Kidijitali hapa nchini, Naibu Waziri wa Fedha, Mh. Hamad Chande amelieleza Bunge jijini Dodoma kuwa, Benki Kuu imebaini kwamba, kama ilivyo kwa mataifa mengi, uanzishwaji wa Sarafu za Kidijitali za Benki Kuu unahitaji kuanzishwa kwa uangalifu na umakini bila kuleta athari hasi katika mifumo ya malipo iliyopo nchini na pia kuweza kutatua tatizo halisi la malipo ambapo kwa sasa bado mifumo iliyopo nchini inakidhi hali halisi ya uwezeshaji mwananchi kutuma fedha na kufanya malipo.
Naibu Waziri Chande amelitaarifu Bunge kuwa, soko letu bado linahitaji kuendelea kuboreshwa katika kuimarisha mifumo iliyopo kwa kutumia vyanzo vinavyopatikana kwa urahisi na wananchi wengi kupitia simu za kawaida tofauti na matumizi ya Sarafu za Kidijitali zinazohitaji matumizi ya simu janja.
Naibu Waziri Mh. Chande ameeleza pia kuwa, nchi nyingi ikiwa ni pamoja na majirani zetu na ukanda wetu bado wapo katika hatua hizi za awali za utafiti na kuboresha mifumo ya malipo iliyopo.