Upotoshaji wa kihistoria wa Humphrey Polepole waibua maswali miongoni mwa wasomi.

Upotoshaji wa kihistoria wa Humphrey Polepole waibua maswali miongoni mwa wasomi.

Na; Mbaruku Fauzi Mbaruku, Zanzibar

Kwa mtu aliyewahi kushika nyadhifa nzito za kidiplomasia akihudumu kama Balozi wa Tanzania katika mataifa zaidi ya moja na pia akishika nafasi ya Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Chama cha Mapinduzi, kufanya kosa la aina hiyo kunafikisha ujumbe wenye uzito mkubwa.

Katika hotuba yake katika siku ya jana kupitia mitandao ya kijamii, Humphrey Polepole alidai kwamba almasi iliyopo kwenye taji la kifalme la Uingereza imetoka Mwadui, Shinyanga.

Kauli hii si tu kwamba si sahihi, bali inaonyesha jitihada za makusudi za kupotosha ukweli ili kuongeza uzito wa hoja zake mbele ya wananchi.

Historia inajulikana wazi kuwa kito cha almasi kinalojulikana kama Kohinoor, kilichimbwa nchini India kati ya karne ya 18 na 19, na kuibwa na mkoloni Mwingereza. Hadi hivi leo, kuna mvutano kati ya India na Uingereza juu ya umiliki wa kito hicho cha thamani.

Kwa mtu kama Humphrey Polepole, ambaye historia yake ya kisiasa na kidiplomasia ilipaswa kumjenga kama mtu makini na msomi. Lakini kitendo cha kutoa kauli kwamba kito cha almasi la taji la kifalme Uingereza kinatoka Mwadui, Tanzania badala ya India, si kosa dogo na la kufumbia macho.

Ni upotoshaji ambao unaacha maswali ya Je, alikosa taarifa? au aliamua kwa makusudi kuupinda ukweli ili kuimarisha hoja yake mbele ya hadhira?

Wasomi wanahoji kwamba kosa la aina hii si tatizo la kitaaluma pekee bali linaweza kupelekea madhara ya kidiplomasia. Katika ulimwengu ambapo mijadala ya urithi wa kikoloni inaendelea, na taifa kama India linaendelea kudai urejeshaji wa Kohinoor, Polepole hakupaswa kusema vile kwa kuzingatia uzito wa nafasi yake na unyeti wa jambo hilo hasa wakati ambao, Tanzania na India ni marafiki wa muda mrefu wenye uhusiano mzuri kidiplomasia na kibiashara.

Wadau na maoni ya watu mbalimbali mtandaoni wanadai kwamba Polopole alidhamiria kudanganya kwa lengo la kuwajaza ghadhabu Watanzania kwa kutumia historia kwa maslahi yake ya kisiasa.

Kwa kauli kama zile, taifa linaweza kupoteza heshima, linaweza kuingia kwenye migongano ya kidiplomasia, na wananchi hubaki wakiwa waathirika wa upotoshaji. Kwa viongozi waliowahi kushika nyadhifa kubwa kama Polepole, kujua historia ya nchi yako na kusema ukweli si hiari, bali wajibu kwa maslahi ya Taifa.