Mashirika ya ndege yaliyoandikishwa nchini Tanzania yanatarajiwa kurejea tena kwenye safari za Ulaya baada ya kukamilisha masharti yaliyowekwa na Umoja wa Ulaya (EU).
Hatua hiyo inakuja kufuatia jitihada mbalimbali zilizochukuliwa na mamlaka za usafiri wa anga nchini, kuhakikisha ndege, wataalamu na mifumo ya usimamizi wa anga inakidhi viwango na taratibu za kimataifa vinavyotakiwa na EU.
Shirika la Ndege la Taifa, Air Tanzania, ndilo linalotarajiwa kuwa la kwanza kuanza safari hizo mara tu taratibu zote zitakapokamilika. Kurejea kwa safari hizo kunatarajiwa kuongeza kasi ya biashara na kukuza sekta ya utalii, ambazo ni nguzo muhimu kwa maendeleo ya uchumi wa taifa.
Taarifa hiyo imetolewa na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), Bw. Abdul Mombokaleo, ambaye alifafanua kuwa marufuku ya awali haikuhusiana na ubora wa ndege za Tanzania, kwani nyingi ni mpya na za kisasa, bali ilikuwa ni kutokana na suala la ulinganifu wa kanuni na taratibu za usimamizi wa anga.
Kurejea kwa safari hizo kunatarajiwa kufungua fursa mpya kwa Watanzania, hususan katika nyanja za biashara, uwekezaji na utalii, huku kikisaidia kuimarisha uhusiano kati ya Tanzania na mataifa ya Ulaya.