Asasi 25 za kiraia Tanzania zilizopokea fedha kutoka Marekani kuchochea machafuko Tanzania

Asasi 25 za kiraia Tanzania zilizopokea fedha kutoka Marekani kuchochea machafuko Tanzania

Taarifa mpya zimeibua mjadala mzito baada ya kubainika kuwa asasi za kiraia 25 nchini Tanzania zimepokea jumla ya zaidi ya shilingi bilioni 21.9 kutoka Ford Foundation ya Marekani, zikidaiwa kutumika katika kufadhili machafuko yaliyotokea October 29, 2025 kwa kivuli cha kupigania demokrasia.

Kwa mujibu wa nyaraka zilizowekwa wazi, fedha hizo zimekuwa zikipokelewa kati ya mwaka 2006 hadi 2025, zikihusisha taasisi na watu binafsi maarufu katika mitandao ya kijamii na kutoka kwenye asasi za kiraira. Miongoni mwa waliotajwa ni mashirika kama Twaweza East Africa Limited, Jamii Forums, Legal and Human Rights Centre, Tanzania Human Rights Defenders Coalition, Tanzania Bora Initiative, na Change Tanzania.

Vilevile, majina ya watu yanayohusishwa moja kwa moja kupokea fedha hizo ni pamoja na Maria Sarungi, Maxence Melo, Onesmo Olengurumwa, Abela Bateyunga, Anna Henga, Tito Magoti, Justice Rutenge, Sema Kilonzo, na wengine kadhaa. Wote hawa wamekuwa mstari wa mbele katika kampeni za kidigitali zinazoshambulia serikali na taasisi zake, hasa katika kipindi cha kuelekea uchaguzi wa mwaka 2025.

Ripoti hiyo inaonyesha kuwa mwaka 2025 pekee, zaidi ya shilingi bilioni 10 ziliingia nchini kupitia asasi tisa za kiraia, ikiwa ni sehemu ya kile kinachoelezwa kama “mpango wa kimkakati wa kujenga mitandao ya ushawishi wa kiraia.” Fedha hizo, kwa mujibu wa taarifa, zilitolewa chini ya majina ya miradi ya “maendeleo ya kidemokrasia” na “ujumuishaji wa wananchi,” lakini maudhui mengi ya miradi hiyo yameelezwa kuwa na mwelekeo wa kisiasa na uchochezi wa kuleta machafuko.

Matokeo ya uchochezi unaofanywa na watu hao, yalijidhihirisha kupitia machafuko ya tarehe 29 Oktoba, yaliyosababisha hasara kubwa za kiuchumi na madhara kwa wananchi wasio na hatia. Licha ya yaliyotokea siku hiyo, taarifa zinaonyesha kuwa wanaharakati hao bado wanaendelea kupanga machafuko mengine ifikapo Desemba 9, wakitumia njia zilezile za mitandao na propaganda za kimataifa.

Taarifa kamili, ikiwemo majina ya mashirika na wahusika wote, imechapishwa kwenye tovuti rasmi ya Ford Foundation, ikiainisha miradi, kiasi cha fedha na mwaka husika wa malipo kwa kila shirika lililohusishwa.