Vikwazo vya Umoja wa Ulaya (EU) vinavyotumika kuendeleza ukoloni mamboleo Afrika.

Vikwazo vya Umoja wa Ulaya (EU) vinavyotumika kuendeleza ukoloni mamboleo Afrika.

Dkt. Albert Samuel Mzindikaya

Katika zama za sasa, ukoloni hauji tena kwa jina la uvamizi, bali umevaa sura mpya ya diplomasia, misaada na vikwazo. Umoja wa Ulaya (EU), ambao kihistoria ulihusika moja kwa moja katika ukoloni wa Afrika, sasa unatumia sera na maamuzi yake ya kiuchumi kudhibiti maamuzi ya mataifa huru ya Afrika kwa jina la “haki za binadamu” na “demokrasia.”

Kwa miaka ya hivi karibuni, Bunge la Ulaya limekuwa mstari wa mbele kuidhinisha vikwazo au kusitisha misaada kwa nchi za Afrika zinazopinga au kutoendana na misimamo ya kisiasa ya Brussels. Mifano kadhaa inaonyesha wazi jinsi vikwazo hivi vinavyotumika kama silaha ya kisiasa badala ya chombo cha maadili.

Nchi kama Zimbabwe, Mali, Niger, na Ethiopia zimewahi kukumbwa na hatua za kusimamishiwa misaada au kuzuiwa mikopo kwa visingizio vya ukiukwaji wa haki za binadamu. Lakini mara nyingi, hatua hizo zimeambatana na mivutano ya kisiasa kati ya serikali za Afrika na nchi wanachama wa EU.

Kwa mfano, Zimbabwe ilipoweka sera ya kurejesha ardhi kwa wananchi wa kawaida, mataifa ya Ulaya yalichukulia hatua hiyo kama tishio kwa maslahi yao ya kihistoria. Mali na Niger zilikumbwa na vikwazo baada ya mapinduzi ya kijeshi, huku raia wao wakibeba gharama ya kiuchumi licha ya changamoto halisi za usalama na ugaidi.

Siku chache zilizopita, Bunge la Ulaya lilipitisha azimio la kupendekeza kusitisha misaada ya Euro milioni 156 (takriban Shilingi bilioni 400) kwa Tanzania kuanzia mwaka wa fedha 2026, kwa kile walichoita “wasiwasi wa haki za binadamu.”

Uamuzi huo umekosolewa vikali kwa kuwa unapuuzia mafanikio makubwa ya kiuchumi na kijamii ambayo Tanzania imepiga chini ya uongozi wake wa sasa, pamoja na ukweli kwamba nchi hii ina bajeti inayojitegemea kwa zaidi ya asilimia 95.

Uchambuzi wa wataalamu wa siasa za kimataifa unaonyesha kuwa vikwazo vya aina hii si vya kusaidia mageuzi, bali ni njia ya kulazimisha utegemezi. Kupitia misaada, mikopo na ushawishi wa kisiasa, EU inaendelea kudhibiti ajenda za ndani za nchi za Afrika – kutoka kwenye sera za uchumi hadi mwelekeo wa kisiasa na diplomasia.

Kimsingi, hii ndiyo sura mpya ya ukoloni mambo leo: si tena kupitia jeshi, bali kupitia taasisi, masharti ya kifedha na vikwazo vya kimaadili vinavyotoka nje ya bara hili.

Wakati mataifa ya Afrika yanajitahidi kujijengea uchumi wa kujitegemea, sera za vikwazo kutoka Ulaya zinaendelea kudhoofisha juhudi hizo. Hii imeibua mjadala mpana kuhusu uhalali wa vikwazo vinavyotolewa na Bunge la Ulaya dhidi ya mataifa huru, bila kujali muktadha wa ndani au vipaumbele vya wananchi wake.

Wataalamu wanasema Afrika inapaswa kusimama pamoja kutetea uhuru wake wa maamuzi, kuimarisha miungano ya kikanda kama Umoja wa Afrika (AU) na Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), na kujenga ushirikiano wa kibiashara unaolinda maslahi yake.

Kwa ujumla, vikwazo vya EU vinabaki kuwa kumbusho kwamba ukoloni haukuisha — umebadilika tu sura. Ni wajibu wa Afrika sasa kuhakikisha inalinda heshima na mamlaka yake bila kuyumbishwa na masharti au vitisho vya misaada kutoka nje.