Mapinduzi ya uchumi wa buluu na hatua ya Rais Samia kuifungua Tanzania kwenye utajiri wa Bahari Kuu.

Mapinduzi ya uchumi wa buluu na hatua ya Rais Samia kuifungua Tanzania kwenye utajiri wa Bahari Kuu.

Uamuzi wa Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kuwa na meli ya kwanza ya uvuvi wa bahari kuu inayomilikiwa na serikali kupitia Shirika la Maendeleo ya Uvuvi nchini (Tanzania Fisheries Corporation – TAFICO) ni hatua ya kimkakati inayobeba sura mpya ya uchumi wa Tanzania.

Hatua hii, ikienda sambamba na mpango wa ununuzi wa meli nyingine nne ambapo mbili kubwa za kisasa zitanunuliwa katika bajeti ya mwaka 2026/27 lengo likiwa ni kuifanya Tanzania kuwa na meli tano za uvuvi wa bahari kuu ifikapo 2030.

Aidha ujenzi wa bandari ya kisasa ya uvuvi Kilwa Masoko uliogharimu shilingi bilioni 280 nao umekamilika. Mradi huu una eneo la ekari 48. Gati iliyojengwa ina urefu wa mita 315 na ina uwezo wa kupaki meli 10 na zikashusha mzigo kwa wakati mmoja. Ina jengo la kuhifadhi tani 1,800 za samaki kwa wakati mmoja na kuzalisha tani 100 za barafu kwa siku ambayo ni mahitaji makubwa ya wavuvi kwa sasa.

Huu si tu uwekezaji wa miundombinu bali ni tangazo la kuingia rasmi katika ushindani wa kimataifa wa uchumi wa buluu.

Fursa ya Rasilimali Iliyokuwa Imelala

Tanzania imebarikiwa na Ukanda wa Pwani wa maji ya Bahari ya Hindi wenye urefu wa kilomita 1,424 na eneo linalojumisha maji ya kitaifa kilomita za mraba 64,000 pamoja na eneo la Ukanda wa Uchumi wa Bahari (EEZ) lenye ukubwa wa kilomita za mraba 223,000
wenye utajiri mkubwa wa samaki wa bahari kuu kama Jodari/Tuna (Yellow fin tuna, Skipjack tuna na Dogtooth tuna), changu, Pweza na uduvi, Kolekole, Blue Marlin, Kaa, na viumbe wengine wa thamani kubwa katika soko la kimataifa.

Kiwango cha samaki wanaovuliwa bahari kuu Tanzania kwa mwaka ni kati ya tani 350,000 na 400,000. Hata hivyo, ukosefu wa meli za kisasa na uwezo mdogo wa kuvua mbali na pwani uliifanya nchi kushuhudia rasilimali hii ikinufaisha zaidi mataifa ya nje kupitia utoaji wa leseni za uvuvi.

Sasa, uwekezaji huu unaashiria mabadiliko kutoka “uchumi wa kukodisha” kwenda “uchumi wa kumiliki na kuzalisha.” Kwa maneno mengine, Tanzania inaanza kuvuna kile ilichokuwa ikikikodisha.

Ajira na Kipato kwa Wananchi wa Kawaida

Kwa mtazamo wa kijamii, athari za uwekezaji huu zitaonekana moja kwa moja kwa wananchi. Meli moja ya uvuvi wa bahari kuu inaweza kutoa ajira za moja kwa moja kwa wafanyakazi 25 – 30 kuanzia mabaharia, wahandisi, wataalamu wa uvuvi hadi wasimamizi wa minyororo ya thamani.

Lakini ajira zisizo za moja kwa moja zitakazozalishwa:-

  • Wasafirishaji wa samaki
  • Wafanyabiashara wa barafu na uhifadhi
  • Wafanyakazi wa viwanda vya kuchakata samaki
  • Wauzaji katika masoko ya ndani na nje

Hii ina maana kwamba mama lishe, vijana na wajasiriamali wadogo watanufaika kupitia mnyororo mzima wa thamani wa sekta ya uvuvi.

Mapato ya Serikali na Fedha za Kigeni

Katika muktadha wa kiuchumi, uvuvi wa bahari kuu ni sekta yenye uwezo mkubwa wa kuingiza fedha za kigeni. Samaki wa aina ya tuna wana soko kubwa katika nchi za Asia, Ulaya na Mashariki ya Kati.

Kwa kuwa na meli zake, serikali itaongeza:-

  • Mapato ya moja kwa moja kupitia mauzo ya samaki nje ya nchi. Kwa sasa Tanzania inauza samaki nje tani 59,000 wenye thamani ya shilingi bilioni 755. Samaki ni kati ya mazao yanayoliingizia Taifa fedha nyingi za kigeni nje ya mazao ya kilimo.
  • Ushuru na kodi kutoka kwa shughuli zinazohusiana na uvuvi
  • Kupunguza utegemezi wa kuagiza bidhaa za samaki kutoka nje. Kwa sasa Tanzania imepunguza uagizaji wa samaki kutoka tani 22,000 hadi tani 9.5 wa samaki aina ya salmon

Hii ni hatua inayochangia kuimarisha mizania ya biashara na kuimarisha thamani ya sarafu ya Taifa kwa muda mrefu.

Bandari ya kisasa Kilwa Masoko ni Kichocheo cha Maendeleo ya Kusini

Ujenzi wa bandari ya kisasa ya uvuvi katika eneo la Kilwa Masoko ni hatua nyingine yenye uzito mkubwa wa kimkakati. Kwa muda mrefu, maeneo ya kusini mwa Tanzania yamekuwa na rasilimali nyingi lakini uwekezaji mdogo wa miundombinu.

Bandari hiyo itakuwa:-

  • Kituo cha kupokelea na kuhifadhi samaki kwa viwango vya kimataifa
  • Kichocheo cha viwanda vya kuchakata samaki
  • Chanzo cha ajira na biashara kwa wakazi wa Lindi na mikoa jirani

Hii ni sehemu ya mkakati wa kuondoa umaskini, kuchochea ukuaji wa uchumi na maendeleo katika kanda ya kusini hususani mkoa wa Lindi kupitia sekta hii ya uvuvi.

Kuimarisha usimamizi wa rasilimali na usalama wa bahari

Umiliki wa meli za serikali pia unaongeza uwezo wa nchi kusimamia rasilimali zake. Mbali na uvuvi, meli hizi zinaweza kusaidia:-

  • Kufuatilia uvuvi haramu (illegal fishing)
  • Kukusanya takwimu sahihi za rasilimali za bahari
  • Kuimarisha uwepo wa Tanzania katika maji yake ya kiuchumi (EEZ)

Hii ni muhimu hasa katika kulinda rasilimali dhidi ya uporaji unaofanywa na meli za kigeni.

Changamoto na Tahadhari

Pamoja na fursa hizi, mafanikio ya uwekezaji huu yatategemea mambo kadhaa:-

  • Usimamizi wenye ufanisi wa Shirika la Maendeleo ya Uvuvi nchini (TAFICO)
  • Uwekezaji katika teknolojia na utaalamu wa kisasa
  • Uwazi na uwajibikaji ili kuepuka hasara au ubadhirifu
  • Ushirikishwaji wa sekta binafsi katika kuchakata na kusambaza bidhaa

Bila kuzingatia haya, hatari ipo ya miradi hii kuwa mizigo badala ya kuwa injini ya uchumi.

Mwanzo wa Safari Mpya

Kwa ujumla, hatua ya Mhe Rais Dkt Samia Suluhu Hassan katika kuwekeza kwenye uvuvi wa bahari kuu si tukio la kawaida, bali ni mwanzo wa safari mpya ya kiuchumi. Ni uwekezaji unaolenga kubadili maisha ya wananchi wa kawaida, kuimarisha uchumi wa Taifa, na kuiweka Tanzania katika ramani ya nchi zinazonufaika kikamilifu na uchumi wa buluu.

Swali kubwa si kama hatua hii ni sahihi bali ni jinsi gani Taifa litaisimamia ili kuhakikisha faida zake zinawafikia Watanzania wote.