Katika kipindi cha hivi karibuni, mjadala kuhusu ongezeko la bei za mafuta umekuwa mkubwa mtaani na katika majukwaa ya kitaifa na kimataifa. Hoja hii si mpya katika historia ya uchumi wa dunia, bali ni mwendelezo wa mizunguko ya misukosuko ya nishati inayochochewa na matukio ya kisiasa, kiusalama na kiuchumi duniani.
Kauli ya Mhe Rais Dkt Samia Suluhu Hassan hivi karibuni kuhusu hatari ya kupanda kwa bei za mafuta kufuatia mivutano ya Mashariki ya Kati imejidhihirisha kwa uhalisia. Mgogoro unaohusisha mataifa makubwa umeongeza taharuki katika masoko ya nishati, na kuathiri moja kwa moja nchi zisizozalisha mafuta kama Tanzania.
Tanzania katika Mfumo wa Soko la Mafuta Duniani
Tanzania ipo katika kundi la nchi “price takers” yaani, haina uwezo wa kuathiri bei za mafuta duniani. Ukosefu wa uzalishaji wa ndani wa mafuta ghafi (haina visima vya mafuta) na miundombinu ya kuchakata unaifanya nchi kutegemea soko la kimataifa, ambako bei huamuliwa na nguvu za uzalishaji, siasa na usalama wa kimataifa.
Historia inaonesha wazi jinsi matukio ya kisiasa yanavyotikisa soko la mafuta. Kuanzia Arab Oil Embargo, hadi Iranian Revolution, na hata vita vya Urusi na Ukraine, misukosuko hii imekuwa na athari za moja kwa moja kwa bei za nishati duniani. Hali ya sasa inaendeleza mtiririko huo huo wa athari.
Gharama za Mafuta ni Zaidi ya Bei ya Soko
Ni muhimu kuelewa kuwa bei ya mafuta kwa mlaji si bei ya soko pekee. Inajumuisha pia gharama za usafirishaji, bima, ushuru na tozo mbalimbali. Katika mazingira ya sasa, gharama za usafirishaji zimeongezeka kutokana na kupanda kwa bei ya mafuta ya meli, pamoja na ongezeko la “war risk premium” katika bima.
Kwa Tanzania, kodi ya mafuta imekuwa chanzo muhimu cha mapato ya maendeleo ikifadhili utekelezaji wa miradi ya barabara, maji, umeme na elimu. Hapa ndipo dhana ya “kupanga ni kuchagua” inapojitokeza: kupunguza kodi kunaweza kupunguza bei kwa muda mfupi, lakini kunaweza pia kupunguza kasi ya maendeleo ya miundombinu na huduma za kijamii.
Kulinganisha Bei na Tahadhari ya Kitaalamu
Mara nyingi, kumekuwa na majaribio ya kulinganisha bei za mafuta kati ya Tanzania na nchi jirani. Hata hivyo, ulinganisho wa aina hii unahitaji kuzingatia vigezo vyote muhimu kama vile viwango vya kodi, ruzuku, gharama za uendeshaji, na hata muda wa kutangazwa kwa bei husika.
Bila kuzingatia “all things being equal,” ulinganisho unaweza kupotosha mjadala badala ya kuusaidia.
Njia za Kimkakati Kupunguza Athari na Kujenga Uhimilivu
Katika kukabiliana na changamoto hizi, Tanzania ina nafasi ya kuchukua hatua za kimkakati ambazo si tu zitapunguza athari za sasa bali pia kujenga uthabiti wa muda mrefu wa sekta ya nishati.
Kwanza, uanzishwaji wa Mfuko wa Kuhimili Bei za Mafuta (Fuel Price Stabilization Fund) unaweza kusaidia kusawazisha athari za mabadiliko makubwa ya bei katika soko la dunia.
Pili, kuanzisha Hifadhi ya Mafuta ya Kimkakati (Strategic Petroleum Reserve) kutaiwezesha nchi kujilinda dhidi ya mishtuko ya ghafla ya ugavi.
Tatu, uwekezaji katika kituo kikubwa cha mafuta (Petroleum Hub) utaongeza uwezo wa kuhifadhi na kusambaza mafuta kwa ufanisi, huku ukiweka Tanzania katika nafasi ya kuwa kitovu cha biashara ya mafuta kikanda.
Nne, utekelezaji wa mfumo wa upokeaji wa mafuta katika ghala moja (Single Receiving Terminal – SRT) kupitia TIPER unaweza kupunguza gharama zisizo za lazima kama demurrage charges na kuongeza uwazi katika biashara ya mafuta.
Tano, kuimarisha taasisi kama TPDC, TBPA na EWURA ni muhimu ili kuhakikisha ufanisi, uwazi na ushindani katika sekta.
Mwelekeo Mpya wa Nishati Ili Kupunguza Utegemezi
Zaidi ya hatua hizo, mustakabali wa Tanzania unategemea uwezo wake wa kupunguza utegemezi wa mafuta. Hapa ndipo uwekezaji katika gesi asilia (CNG), nishati jadidifu (vyombo vya usafiri vinavyotumia umeme), na ubunifu wa teknolojia unakuwa muhimu.
Kuongeza vituo vya CNG na kutoa motisha za kikodi kwa watumiaji kunaweza kubadilisha kwa kiasi kikubwa muundo wa matumizi ya nishati nchini. Hii si tu itapunguza gharama kwa wananchi, bali pia itaimarisha usalama wa nishati wa Taifa.
Aidha, kupanua wigo wa kodi na kukuza uchumi unaozalisha kutapunguza utegemezi wa mafuta kama chanzo kikuu cha mapato ya serikali kwa ajili ya miradi ya maendeleo.
Mtazamo wa Kikanda na Kimataifa
Katika dunia inayobadilika kwa kasi, ushirikiano wa kikanda ni muhimu. Kuingia makubaliano na nchi zinazozalisha mafuta barani Afrika kama Nigeria, Angola na Namibia kunaweza kupanua vyanzo vya ugavi, kutuepusha na athari za mitikisiko wa kiusalama duniani pamoja na kupunguza hatari ya utegemezi kwa masoko machache.
Hitimisho: Tanzania Imara ya Kesho
Changamoto ya bei za mafuta si ya muda mfupi, bali ni sehemu ya mabadiliko ya kimfumo katika uchumi wa dunia. Kwa Tanzania, hii ni fursa ya kuongeza kasi na kuendelea kufanya mageuzi ya kimkakati kujenga uchumi unaostahimili mishtuko, unaotegemea vyanzo mbalimbali vya nishati, na unaochochea maendeleo endelevu..
Kupitia uongozi thabiti na utekelezaji wenye nidhamu chini ya Mhe Rais Dkt Samia Suluhu Hassan, Tanzania inaweza kubadilisha changamoto ya leo kuwa msingi wa uimara wa kesho.
