BOT: Matumizi ya noti ya 10,000 yameongezeka kwa 75%, hii ina maana gani kwenye uchumi?

BOT: Matumizi ya noti ya 10,000 yameongezeka kwa 75%, hii ina maana gani kwenye uchumi?

Gavana wa Benki Kuu nchini Tanzania Emmanuel Tutuba amesema kwamba kuongezeka kwa matumizi ya noti ya Tsh 10,000 ni ishara ya kwamba uchumi unazidi kufunguka na biashara zinaongezeka.

Gavana Tutuba amesema, matumizi ya noti ya Tsh 10,000 yameongezeka kwa asilimia 75 ndani ya miaka mitano.

Takwimu za Benki Kuu Tanzania zinaonesha mzunguko wa noti ya 10,000 kwa mwaka 2018 ulikuwa ni Tsh trilioni 3.6 na hadi kufikia mwishoni wa Desemba 2023 mzunguko huo ulikua hadi Tsh trilioni 6.3.

Kwa mujibu wa Gavana, hii ni ishara ya kufunguka kwa uchumi pamoja na kukua kwa biashara, hali ambayo imechangiwa na serikali kuweka mazingira mazuri na ya wazi ya kufanyia biashara nchini.

Gavana Tutuba pia ameongeza kwamba mfumuko wa bei sio sababu kuongezeka kwa mzunguko huo kama wengi wasemavyo, kwani mwaka wote 2023 Tanzania imefanikiwa kudhibiti mfumuko wa bei chini ya asilimia 3.