Makunduchi, Unguja – Mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Samia Suluhu Hassan, amewahakikishia Watanzania kuwa vyombo vya ulinzi na usalama vipo imara na vimejipanga kikamilifu kuhakikisha Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025 unafanyika kwa amani na utulivu.
Akizungumza jana Septemba 17, 2025 katika Kijiji cha Kajengwa, Makunduchi – Unguja, Dkt. Samia alisema amejikita kuimarisha misingi ya amani kwa kuwa amani ni nguzo muhimu ya maendeleo na ustawi wa Taifa. Alisema kauli hiyo imetokana na maombi ya wazee wa Pemba waliomweleza umuhimu wa kulinda utulivu wakati wa uchaguzi.
“Ninawaomba sana twende tudumishe amani na utulivu. Uchaguzi siyo vita, bali ni tendo la kidemokrasia – wananchi kwenda kwenye vituo, kuweka kura zao na kurejea nyumbani kwa amani. Silaha hazijawahi kuleta suluhu ya maana. Amani na utulivu wa nchi yetu ni jambo muhimu kuliko jambo lolote,” alisema Dkt. Samia.
Akitaja historia yake kama mwanamke wa kwanza kupewa ridhaa na CCM kugombea urais, Dkt. Samia alisisitiza dhamira yake ya kuendelea kuongoza nchi kwa misingi ya mshikamano na utulivu, akisema kuwa jukumu la kudumisha amani ni la kila Mtanzania.