KIGOGO2014 (DIDIER MLAWA): KUTOKA UANAHARAKATI WA MTANDAONI HADI UTAPELI

KIGOGO2014 (DIDIER MLAWA): KUTOKA UANAHARAKATI WA MTANDAONI HADI UTAPELI

Kuanzia mwaka 2019, jina Kigogo2014 lilijipatia umaarufu mkubwa na wafuasi wengi wa mtandaoni nchini Tanzania. Kigogo2014 ambaye jina lake halisi ni Didier Mlawa alijizolea umaarufu huo kwa machapisho yake ya utetezi wa demokrasia, haki za binadamu na ubadhirifu chini ya utawala wa Rais John Magufuli. Uanaharakati wake huo ukamjengea maadui wakubwa kwenye utawala wa Magufuli ikabidi aikimbie Tanzania na kupewa hifadhi ya ukimbizi nchini Uingereza. Kwa mujibu wa sheria za Uingereza, kiasi fulani cha fedha zake za kujikimu na kodi ya nyumba anakipata kutoka katika ruzuku ya serikali ya nchi hiyo ambayo kimsingi ni fedha za walipakodi wa Uingereza. Mbali na Uingereza, amepokea pia misaada kutoka shirika la Marekani la Ford Foundation.

Machi 17, 2021 Tanzania ilikumbwa na msiba mkubwa kitaifa Rais John Magufuli alipofariki akiwa madarakani. Siku mbili baadaye, Machi 19, Makamu wake, Samia Suluhu akaapishwa kuwa Rais na mambo yakaanza kubadilika. Rais mpya akaanza mazungumzo na wapinzani, akawatoa wengine gerezani na kuwafutia mashtaka. Wafanyabiashara ambao nao walikuwa wameteswa na kukwapuliwa hela zao wakati wa Magufuli pasi haki wakarudishiwa amana zao. Mikutano ya hadhara ya vyama vya siasa pia ikaruhusiwa tena. Kutokana na hatua hizi za Rais mpya kuipa nchi uponyaji wa kisiasa na haki, waliokuwa wameikimbia Tanzania wakaanza kurudi.

Hata hivyo licha ya maendeleo hayo mazuri kwenye haki za kibinadamu ambayo Rais Samia alikuwa ameanza kuonesha, Mlawa aliendelea kuipinga serikali ya Tanzania kama vile hakuna lililokuwa limebadilika. Mtazamo wake huo ukadumu kwa miezi michache kisha ghafla akaanza kuwa mtetezi wa serikali. Kutokana na umaarufu aliokuwa nao mtandaoni, kubadilika kwake huku kukaonekana kama usaliti na kuwa amefika bei na kununuliwa na serikali na wanasiasa Tanzania.

Licha ya kubadilika na kuwa mtetezi wa serikali, Mlawa hakurudi rasmi Tanzania kama vile ambavyo wakimbizi wenzake wa kisiasa walikuwa wanafanya na badala yake akaanza kuja Tanzania kisiri. Toka Rais Samia aingie madarakani, Mlawa amefika Tanzania mara tatu. Mara zote tatu amekuwa akikutana na wanasiasa mbalimbali, wafanyabiashara na viongozi wa serikali. Katika mikutano hiyo amekuwa anauza “kukusemea vizuri” mitandaoni kama bidhaa kwa kiasi kikubwa cha fedha. Unamlipa kukusema vizuri kwenye mitandao, kukupamba na pia kuwasemea vibaya mahasimu wako kwa propaganda mbalimbali.
Hata hivyo, wachambuzi wanauliza inakuwaje Mlawa anakuwa na uthubutu wa kuingia Tanzania nchi ambayo aliondoka na kuomba hifadhi Uingereza akisema si salama kwake? Je! Uingereza inachukuliaje mwenendo wake huu?

Jibu ni hilo kwamba amekuwa akiingia nchini kwa kificho, kuwaficha Idara ya Uhamiaji ya Uingereza kwamba haji Tanzania bali Kenya. Anachofanya ni kuwa huaga Uingereza kuwa anakwenda Kenya. Akifika Kenya anachukua usafiri wa gari na kuvuka mpaka wa Kenya na Tanzania mara nyingi mpaka wa Horohoro mkoani Tanga. Anapovuka mpaka huwa hagongi muhuri katika pasipoti ili asionekane alikuja Tanzania. Baadhi ya wanaharakati wanaona jambo hili na utapeli mkubwa na uhalifu na sasa wanaishinikiza Idara ya Uhamiaji ya Uingereza kumfutia Mlawa hisani ya ukimbizi kuishi nchini Uingereza. Shirika la Marekani la Ford Foundation ambalo awali lilikuwa likimpa misaada tayari limemuondoa katika orodha yake ya wanufaika. Awali lilimpa msaada wa zaidi ya dola 15,000 (shilingi milioni 35).

Safari yake ya mwisho kuja Tanzania ilikuwa Januari mwaka huu kama ifuatavyo; Januari 5 mwaka huu aliondoka katika uwanja wa ndege wa Heathrow London akiwa abiria kwenye ndege namba QR006 ya shirika la Qatar Airways kuelekea Doha. Doha akabadili ndege na kuelekea Nairobi, Kenya, ndege namba QR1335 ya shirika hilo hilo. Alitua Nairobi Januari 6 saa moja na dakika 20 asubuhi. Kutoka Nairobi alitumia usafiri wa gari binafsi na kuvuka mpaka wa Horohoro, Tanga kisha kuingia Tanzania, bila kugonga pasipoti muhuri mpakani. Alikuja moja kwa moja hadi Dar es Salaam na kati ya tarehe 7 hadi 13 mwezi huo huo wa Januari alifanya mikutano ya kificho na wanasiasa na viongozi mbalimbali. Baada ya mikutano hiyo akarudi tena Nairobi kwa barabara. Nairobi akapanda ndege ya shirika la Qatar kurudi Uingereza kwa kupitia Doha. Aliondoka Nairobi tarehe 14 Januari saa nne usiku katika ndege namba QR005.

Katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita Mlawa (Kigogo) amejibadili toka kuwa mwanaharakati hadi kuwa tapeli na mhalifu wa mtandaoni. Mfano katika akaunti yake rasmi ya Twitter ya Kigogo2014 amejitangaza kwamba anazisemea vizuri kazi za Rais Samia Suluhu. Hata hivyo, uchunguzi unaonesha anazo akaunti zaidi ya 100 zikiwemo TanzaniaLeaks, Insightfactortz na Tanzania Whistleblowers Group ambazo amekuwa akizitumia kumshambulia Rais Samia, familia yake na serikali ya Tanzania. Utaratibu wake ni kwamba akishakushambulia katika akaunti hizo kwa propaganda huja kwa mlango wa nyuma na kuwaomba watu hao hao wampe fedha ili azishughulikie akaunti hizo ikiwemo kuzidukua kana kwamba si zake. Vyanzo vinaeleza kwamba huchukua kati ya shilingi milioni 10 hadi 50 na zaidi kwa vitendo hivyo ambavyo kimsingi ni uhalifu dhidi ya wahanga wake.

Pia anatoa huduma za kuwasemea vibaya maadui za wanasiasa. Anachofanya ni kupendekeza kwako kwamba fulani ni adui, au kupata taarifa za fulani ni adui yako kisha hukuomba fedha ili aweze kueneza propaganda na uongo dhidi ya huyo adui yako kisiasa au kwenye biashara. Mbali na haya, amevujisha pia taarifa nyingi za wanaharakati aliokuwa akifanya nao kazi na baadhi hivi sasa wanahofia uhai wao.

Ni dhahiri kwamba Kigogo sasa anajiingizia fedha kutoka kwa kazi hii aliyochagua na hatahitaji hisani ya kuishi Uingereza kwa msaada za walipakodi wa nchi hiyo. Pengine ni wakati sasa wa vyombo vya ulinzi na usalama vya Tanzania na Uingereza kuanza uchunguzi juu ya Mlawa ili hatua zichukuliwe ikiwemo Uingereza kumfutia hadhi ya ukimbizi wa kisiasa inayompa haki ya kuishi nchini Uingereza hivi sasa. Ni wakati pia wa umma kumpuuza jambo ambalo lilianza pale tu ilipoonekana wazi amenunuliwa na serikali.

Imran Mjanenga
Safarini Dodoma Tanzania
imjanenga@gmail.com