- WAZIRI wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, January Makamba, amesema ziara za Rais Samia Suluhu Hassan zimeiwezesha nchi kupata miradi ya zaidi ya USD bilioni 5.6 na mtaji unaoingizwa nchini kukua kutoka USD Bilioni 1 moja mwaka 2020 hadi USD Bilioni 5.6 mwaka huu.
Akizungumza katika mahojiano maalum na waandishi wa habari wa kampuni ya The Guardian Limited kuhusu miaka mitatu ya Rais Samia madarakani, Makamba amesema miradi mingi ni yenye kubadilisha maisha ya Watanzania na kukuza uchumi wa nchi.
“Hizi ziara zina manufaa makubwa na ya moja kwa moja, mfano hivi karibuni alienda Morocco kwenye mkutano wa African Investment Forum, ambako alikuwa na mazungumzo ya miradi mingi duniani.
Lakini alikuwa na miradi yake ambayo ni Bandari ya Mangapwani Zanzibar, reli mpya kutoka Ziwa Nyasa Mbaba Bay hadi Songea, Mchunguma hadi Mtwara.
“Alikuja na mradi wa kipande cha SGR Kigoma hadi Burundi na kwamba ilipokelewa na kupata fedha kwa mikopo nafuu.
Nina mifano mingi sana ya Rais Samia anavyokuwapo kwenye mikutano anawezesha upatikanaji wa fedha za miradi mingi kwa ajili ya nchi. Kwa safari hii moja tulipata miradi ya Sh. bilioni sita,” amesema.
Kwa mujibu wa Makamba, kila wanapofanya ziara nje ya nchi wanakutana na wawekezaji, wanafanya kongamano la biashara la uwekezaji na lengo ni kuhakikisha nchi inanufaika.
“Mfano mwaka 2020 kiwango cha mtaji ulioingia hapa nchini ulikuwa Dola bilioni moja, lakini mwaka jana tumeingiza Dola bilioni 5.6, kutokana na ushawishi wa yeye kwenda, wawekezaji kubwa duniani wanachohitaji ni kumuona Rais, kumsikia, kumtazama usoni na kumsikia kauli yake basi,” amesema.
Waziri Makamba ambaye ni Mbunge wa Bumbuli alisema viongozi wengi wanaweza kwenda na kuzungumza, lakini watu wanaamini sana mkiwa na Rais, ndio maana kiwanda cha mtaji kilichoingia kimeongezeka.
“Safari hizi hii ina maana gani? Mapato ya serikali yameongezeka ambayo yatawezesha kujenga zahanati, kuchonga barabara, elimu bure, kufikisha umeme vijijij, kutengeneza madawati na kununua dawa zaidi. Mfano biashara kati ya India na Tanzania ilikuwa inasuasua, tumeenda kule Rais ametoa ushawishi na sasa mbaazi nyingi inanunuliwa.
“India inalima mbaazi pia, hivyo inatoa nafasi ndogo kwa baadhi ya nchi na kwamba kuwa ziara ya Rais Samia sasa tunauza mbaazi nyingi na wananchi maisha yao yamebadilika na kununua vyombo vya usafiri, kujenga nyumba zao na kuhudumia familia zao. Utaona kuna faida ya moja kwa moja kutokana na ushawishi.
“Watu wengi hawajui kwamba hakuna hata nafasi ya kupumua tunaposafiri, anatoa mkutano huu na kwenda mwingine, akifika kwenye ndege amechoka (Rais Samia) kabisa. Sisi tunaona manufaa makubwa sana na wakati mwingine tunatamani twende naye kila mahali kwa sababu kazi inakuwa rahisi zaidi,” amesema.