Licha ya vivutio vingi duniani kukumbwa na uhaba wa wageni, Tanzania imeendelea kushuhudia ongezeko kubwa la watalii kwenye vivutio vyake mbalimbali nchini.
Haya yote yamewezekana kutokana na ubunifu mahiri wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh. Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambaye ametenga muda wake binafsi kwa ajili ya kuvitangaza vivutio vya utalii vya Tanzania kupitia filamu maarufu duniani ya Royal Tour, aliyoshiriki kama mhusika mkuu wa kuvielezea vivutio na fursa za utalii nchini.
Kupitia filamu hiyo iliyojizolea umaarufu duniani kote baada ya kuzinduliwa nchini Marekani na hapa Tanzania, sekta ya utalii iliyokuwa inapitia changamoto za kukosa wageni, kupoteza ajira, kushuka kwa mapato yaliyokadiriwa kuingia serikalini na mdororo wa mzunguko wa fedha katika jamii, ilifufuka na kuanza kurudia hali yake ya mwanzo.
Inakadiriwa kuwa takribani watalii 1,527,230 waliingia nchini mwaka 2019/20. Idadi hiyo ni ndogo sana ukilinganisha na watalii 1,808,205 waliorekodiwa kuingia nchini mwaka 2023. Ongezeko hilo ni sawa na asilimia 8.09 ya lengo la watalii 5,000,000 ifikapo mwaka 2025/26.
Mchango mkubwa wa Mh. Dkt. Samia Suluhu Hassan umepelekea kuongezeka kwa mapato yatokanayo na utalii kutoka dola za kimarekani bilioni 2.6 mwaka 2019/20 hadi kufikia dola za kimarekani bilioni 3.4 mwaka 2023/24. Hilo limetajwa kuwa ongezeko la asilimia 23, ikiwa ni sehemu za jitihada za kuifikia malengo ya kitaifa ya kufikia dola za kimarekani bilioni 6.0 ifikapo 2025.
Hatua hizi zimeirudisha Tanzania katika nafasi za juu zaidi barani Afrika zinazopokea watalii wengi. Matokeo yake kwa Watanzania ni mfumuko wa ajira zilizoongezeka kupitia utalii, ongezeko la fedha za kigeni na tumaini jipya kwa taifa kiuchumi.
Shauku ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imekuwa pia kuhamasisha utalii wa ndani hasa kwa vijana na watoto wadogo ili wajue na kuelewa nafasi ya utalii kwa ukuaji na ustawi wa taifa letu kiuchumi. Hatua mbalimbali kama kupunguza bei kwa Watanzania kuingia kwenye mbuga za wanyama zimeendelea kuchukuliwa ili kuhamasisha wazawa wengi zaidi kuzuru maeneo mbalimbali yenye vivutio.