Nini Kinaendelea CHADEMA?

Nini Kinaendelea CHADEMA?

Dhana iliyozungumziwa kwa muda mrefu kwamba FREEMAN MBOWE Kalambishwa asali sasa ni dhahiri baada ya Mr. Mbowe kuanza kusambaza kiasi kikubwa cha fedha kwenye chaguzi tofauti tofauti nchi nzima ndani ya chama chake cha Chadema, kwa malengo ya kupanga safu yake ya 2025.

Kilichotokea kwenye uchaguzi wa kanda ya Nyasa imeshtua wengi hasa wajumbe waliopiga kura baada ya kamati ndogo inayoundwa na Mbowe, ikijumuisha Susan Kiwanga, Meiseyeki Gibson na Abokile Mwaitenda kuingilia Chaguzi kwa minajili ya kuwaondoa wote wenye misimamo mikali kama Lissu, Lema, Msigwa, Heche , Catherine Ruge nk.

Lengo kubwa la kufuta uchaguzi wa Nyasa ni kumuondoa Msigwa ambaye anaonekana kuwa na msimamo mkali. Baada ya kuyaona yanayomsibu Msigwa, Heche amegoma kuchukua fomu ya kuwania uenyekiti kanda ya Serengeti . Mfano ni huu upuuzi alioufanya mkoa wa Njombe na Iringa. Ambapo kundi la Mbowe limefuta uchaguzi wa Njombe. Huku uchaguzi wa Iringa ukiingiliwa na polisi walioitwa na timu ya Mbowe baada ya kuona kibaraka wa Mbowe, William Mungai anaenda Kushindwa vibaya.

Lengo la kuvuruga chaguzi hizi, ni kutafuta namna ya kumbeba Sugu ambaye ni Kibaraka wa Abdul mtoto wa Rais Samia. Sugu anaonekana kutokuwa na kura za kutosha kanda ya Nyasa.

Tunavyoongea, katibu mkuu wa CHADEMA John Mnyika, ameamua kukaa kando kupisha huu uchafu unaoendelea. Hataki kuwa sehemu ya huu uhuni. Ila Lissu kaamua kufyatuka, na waraka wake ni huu hapa chini bila kuongeza wala kupunguza.

Kadhalika tumeambatanisha waraka wa siri uliosainiwa na wajumbe 40 waliopiga kura Kanda ya Nyasa. Kadhalika tunaambatanisha barua ya kuufuta uchaguzi huo, ambao ulistahili kusainkwa na John Mnyika, lakini Mnyika Kagoma kuwa sehemu ya uchafu wa Mbowe. Kwa maana hiyo mkoa wa Njombe hauna uongozi wowote na tarehe ya uchaguzi haujatangazwa.

UJUMBE WA LISSU KWENDA KWA WAJUMBE KAMATI KUU HUU HAPA CHINI

Wajumbe wa Kamati Kuu salaam. Nimepokea barua hiyo kutoka viongozi wetu wa Njombe. Barua yenyewe inajieleza na mnaweza kuisoma na kuielewa wote. Pamoja na kwamba haijatumwa kwa wajumbe wote wa Kamati Kuu, sidhani kama ni sawa sawa kwangu kuikalia kimya.

Ukweli ni kwamba masuala haya yanafahamika humu, hata kama ni kwa njia zisizo rasmi. Kamati Kuu ni chombo cha chama chenye mamlaka makubwa kikatiba.

Lakini mamlaka hayo yana mipaka yake, sio unlimited. Mipaka hiyo ni Katiba yenyewe ya Chama na sheria za nchi hii. Kuna baadhi yetu tunaamini kwamba chochote kinachofanywa na sisi Kamati Kuu ni halali, bila kujali Katiba yetu inasema nini.

Baadhi yetu tunajificha nyuma ya maamuzi ya vikao vya Baraza Kuu, bila kujali mamlaka ya kikatiba ya Baraza Kuu kuhusu maamuzi hayo, na kufanya maamuzi tutakavyo sisi. Hii sio tu sio sahihi kikatiba, ni hatari kwa chama chetu. Kwenye chaguzi zinazoendelea kila mahali, secretariat ya Kamati Kuu na baadhi ya wajumbe wa Kamati Kuu, wamefanya maamuzi mengi na makubwa.

Kimsingi, wajumbe wa secretariat wameendesha chaguzi za chama karibu katika ngazi zote hadi sasa.

Wajumbe wa secretariat wamepangua na kupanga safu za uongozi wa chama; wameengua wagombea wasiowataka kwa vigezo vyao wenyewe; wametengua maamuzi ya vikao halali vya chama wasiyoyataka; wameamua rufaa zilizotokana na maamuzi yao wenyewe, n.k.

Naomba tuulizane: je hivyo ndivyo Katiba yetu inavyotaka???

Malalamiko juu ya matendo haya ni mengi ajabu na yapo kwenye Kanda karibu zote. Ninaamini wajumbe wa Kamati Kuu mnayafahamu malalamiko haya, kama tunavyoyafahamu tulio viongozi wakuu wa chama.

Suala linalonitatiza mimi ni kwa nini tumeamua kuyaruhusu au kuyanyamazia. Tunayaruhusu au kuyanyamazia kwa ajili ya maslahi ya Chama kweli au ni kwa ajili ya maslahi mengine tusiyoyajua wengine.

Kumekuwa na matumizi ya nguvu kubwa sana, ya kifedha na kimadaraka, katika chaguzi hizi. Chama chetu kina matatizo makubwa ya fedha za uendeshaji wa shughuli za chama katika ngazi zote za chama.

Lakini katika chaguzi hizi kumekuwa na fedha nyingi ajabu. Mimi najiuliza hizi ni fedha zetu wenyewe, au ni fedha za Abduli na mama yake???

Fedha ni muhimu sana katika maisha ya binadamu na katika uendeshaji wa shughuli za chama. Lakini ni kweli pia kwamba sio kila pesa tunayoihitaji au kuitumia ni pesa halali, na sio kila matumizi hayo ni matumizi halali.

Tusije tukasahau kwamba pesa ndiyo iliyomuuza Yesu kwa watesi wake, na pesa ndiyo mojawapo ya silaha kubwa za maangamizi zinazotumiwa na watesi wa wananchi wetu na watesi wetu wenyewe miaka yote.

Tusije tukasahau maneno ya Mwenyekiti wetu kwamba katika vitu vyote vinne vinavyohitajika kushinda uchaguzi (au kuendesha chama) – wagombea, agenda, oganaizesheni , pesa – pesa ni hitaji la mwisho kabisa.

Sasa, kwa kinachoendelea kwenye chaguzi hizi, pesa inaelekea kuwa ndio hitaji la kwanza. Na tunaelekea kuamini kuwa pesa ni pesa, hata kama ni ya Abduli na mama yake.

Tusipokataa utamaduni huu mpya kwenye chama chetu, pesa hizi zitatutokea puani. Zitatuchafua na kutuharibia chama, kama ambavyo zimewachafua na kuwaharibia wa vyama vingine tunaowafahamu vyema.

Nawaombeni tusikubali uchafu huu kwenye chama chetu. Nawaombeni haya yanayoendelea kwenye chama kwenye chaguzi hizi tuyazungumze kwa undani na kwa uharaka unaohitajika.

Tusikubali kutishwa na kutishana hata humu kwenye Kamati Kuu. Tunaangaliwa, sio tu na watesi wetu wanaotutakia maafa, bali pia na wapenzi wetu wanaotutakia mema.

Tusikubali kukumbatia au kunyamazia uovu kwa sababu tu uovu huo umefunikwa na pesa au na madaraka. Nawaombeni tuyazungumze haya kwenye kikao rasmi cha Kamati Kuu.
Tundu Lissu