Jeshi la Polisi limeibua madai mazito dhidi ya viongozi wa CHADEMA, likidai kuwa wamepanga njama za kuvuruga amani nchini kupitia vitendo vya uhalifu. Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Polisi, viongozi hao walifanya mkutano kwa njia ya mtandao (Zoom) ambapo walikubaliana kuhamasisha wafuasi wao kufanya maandamano ya vurugu na kushambulia ofisi mbalimbali.
Taarifa hiyo inaeleza zaidi kuwa viongozi wa CHADEMA walipanga kuunda vikundi vya vijana wapatao 20 kwa lengo la kuvamia vituo vya polisi jijini Dar es Salaam kwa wakati mmoja, hatua ambayo Polisi wanasema inahatarisha usalama na amani ya nchi.
“Jeshi la Polisi linatoa onyo kali kwa yeyote anayehusika na njama hizi za uhalifu na vurugu,” inasomeka sehemu ya taarifa hiyo. “Tumejiandaa kikamilifu na yeyote atakayejaribu kuvuruga amani au kufika katika kituo cha polisi kwa nia ovu, atakutana na mkono wa sheria.”
Jeshi la Polisi limeongeza kuwa hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi ya wote watakaoshiriki katika uhalifu huo, na kuwataka wananchi kushirikiana na vyombo vya usalama ili kudumisha amani nchini.