Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan yupo nchini Zimbabwe kuhudhuria Mkutano wa 44 wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) utakaofanyika tarehe 17 Agosti 2024 jijini Harare, Zimbabwe.
Katika Mkutano huo, Rais Samia anatarajia kuchaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya SADC. Rais Samia anapokea kijiti hicho kutoka kwa Rais wa Jamhuri ya Zambia Mhe. Haikande Hichilema.
Kauli mbiu ya Mkutano wa mwaka huu ni “Kukuza ubunifu ili kufungua fursa za ukuaji wa uchumia na maendeleo endelevu kuelekea SADC yenye viwanda”.
Uongozi wa Rais Samia kwenye Asasi hiyo unatarajia kuangazia utulivu wa kisiasa na kudumisha mahusiano mazuri kati ya nchi wanachama. Rais Samia pia anatarajia kuongoza jitihada za pamoja za uimarishwaji wa vikosi vya pamoja na makabiliano dhidi ya makundi ya waasi, biashara haramu, na makundi ya kigaidi.
Katika dhima ya ukombozi wa kiuchumi kwa nchi zinazoendelea, maendeleo endelevu yenye kuhusisha uanzishwaji wa viwanda ni nyenzo muhimu ya kuchochea uchumi. Nafasi ya Asasi ya Siasa, Ulinza na Usalama ni kuhakikisha uwepo wa mazingira mazuri ya kisiasa yanayoshawishi wawekezaji juu ya ulinzi na usalama wa mali zao.
Rais Samia ameendelea kuwa na mchango usiomithilika kwenye uwanda wa utawala na uongozi bora, hali inayoakisi kuaminika mpaka nje ya mipaka ya Tanzania.