Ili kuendana na hali ya sasa ya mabadiliko ya teknolojia, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imedhamira kufanya maboresho kwenye Sheria za Makampuni sura 212 ya Majina ya Kampuni, lengo kuu likiwa ni kukuza na kuvutia uwekezaji zaidi nchini.
Uamuzi huo umechukuliwa baada ya wadau wa biashara nchini kutuma maoni yao kwa Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELLA), wakidai sheria hiyo haiendani na mazingira ya sasa ya biashara nchini.
BRELA baada ya kupokea maoni ya wadau, ni kweli iligundua dosari kwenye sheria hizo ikiwemo masharti ya kuwa ili upate jina la biashara basi ni lazima iwe na watu 20 na iwe na majukumu tofauti manne, wadau walipendekeza kampuni iwe na kazi moja na idadi ya watu ipunguzwe kutoka 20.
Brela imefanya jukumu lake kikamilifu na kisha kuyapeleka kwenye tume ya mabadiliko ya sheria kwa kufanyiwa kazi zaidi.
Akichangia mjadala wa mabadiliko ya sheria hiyo Machi 12, 2024 jijini Dar es Salaam, Balozi Mwanaidi Majaar amependekeza Sheria ya Makampuni namba 400A iondolewe.
Amesema sheria hiyo inampa mamlaka makubwa msajili wa kampuni yoyote bila kujiridhisha, inapotuhumiwa kwa masuala ya uhalifu.
“Msajili hawezi jua kwenye kampuni fulani umetendeka uhalifu bila uchunguzi wa vyombo vya usalama, hakuna utaratibu unaofuatwa, bali ni kampuni kufutwa, sasa kama sheria hii mliweka muwatishe wahalifu, basi mmefukuza watu wazuri, tanataka kuwe na sheria ya kuwalinda wafanyabiashara dhidi ya tatizo lolote linapotokea, hatua zichukuliwe kwa kosa lisilotiliwa shaka,” amesema.
Kwa upande wa Mtendaji Mkuu wa Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania, Nathaniel Mandepo amesema maboresho yatakayofanyika ni katika kutengeneza mazingira ya uwekezaji.
“Hatua hizi za awali za kukusanya maoni ya wataalamu inafuatana na. utafiti wa mapungufu kwenye sheria, sera na mfumo unaotumia sheria husika, kupata taarifa muhimu zinatazosaidia maboresho,” amesema.
Naye Mkurugenzi wa Usajili Makampuni na Majina ya Biashara BRELLA, Isdor Nkindi amesema baada ya maboresho ya sheria ya wafanyabiashara na wanajamii watajiona ni wadau wanaotegemeana.
“Kampuni zinazorudisha mchango kwa jamii (CSR) zimekuwa zikiona zinachokifanya ni hisani, hivyo sheria itakwenda kutambua CSR kama takwa la kisheria. Kwa mataifa mengine CSR ni jambao la lazima,” alisema.