Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, imedhamiria kuchochea ongezeko kubwa la vipaji vya michezo nchini, hususan vya mpira wa miguu. Lengo la Serikali ni kutengeneza vipaji vingi vyenye ubora mkubwa wa kutumika hapa nchini na kwengineko duniani hasa nchi zilizoendelea kisoka barani Afrika na Ulaya.
Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mh. Hamis Mwinjuma ameyasema hayo bungeni jijini Dodoma alipokuwa akijibu swali la mbunge wa jimbo la Geita Mjini Mh. Constantine Kanyasu aliyetaka kufahamu kuna mkakati gani wa kutengeneza vipaji vya wachezaji wa mpira wa miguu nchini.
Naibu Waziri Mwinjuma amelihakikishia bunge kuwa kuna ushirikiano kati ya Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo na Shirikisho la soka nchini (TFF) na wadau wengine mbalimbali katika kuratibu na kusimamia programu mbalimbali za kutengeneza vipaji vya wachezaji wa mpira wa miguu.
Hii kwa mujibu wa Naibu Waziri Mwinjuma, inajumuisha uanzishwaji wa vituo vya kulea vipaji vya michezo, kuratibu ligi na mashindano ya kimataifa kwa vijana ya U20 na U17, kuratibu na kushiriki mashindano ya kimataifa ya shule (CAF African School Football Championship) na kupeleka vijana wenye vipaji kwenye vituo vya kulea vipaji vya michezo nje ya nchi.
Akifafanua zaidi kupitia majibu yake ya swali hilo la mbunge wa Geita Mjini, Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mh. Mwinjuma, alieleza pia kuwa, Wizara kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais- TAMISEMI na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imetenga jumla ya shule 56 za sekondari katika mikoa yote kwa ajili ya kukuza na kulea vipaji vya michezo mbalimbali ikiwemo mpira wa miguu pamoja na kuendelea kuratibu mashindano ya UMITASHUMTA na UMISSETA ambapo wachezaji watakaofanya vizuri watapelekwa kwenye timu za Taifa za U20 na U17 kwa ajili ya kuendeleza vipaji vyao kila baada ya mashindano hayo.
Akihitimisha majibu yake, Naibu Waziri, Mh. Mwinjuma amelieleza bunge kuwa, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya uongozi shupavu wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, inaamini kwamba itafanikiwa kuibua, kukuza na kuendeleza vipaji vya wachezaji wa mpira wa miguu nchini na hatimaye kuwa na timu ya Taifa yenye uwezo wa kushindana kimataifa na kuleta heshima kwa nchi yetu.