Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeendelea na dhamira yake ya kuhamasisha uwekezaji nchini, kwa kuongeza kasi ya uwekaji mazingira rafiki katika sekta mbalimbali nchini.
Kupitia Kituo cha Uwekezaji nchini (TIC), Serikali imeanza kutafuta muwekezaji kwa ajili ya kilimo cha miwa na kiwanda cha sukari wilayani Kilolo, Iringa.
Kufuatia maelekezo ya Serikali, Bodi ya sukari nchini imeshafanya upembuzi wa awali uliojikita kubaini maeneo yanayofaa kwa kilimo cha miwa na uwekezaji wa viwanda vya sukari katika wilaya ya Kilolo, mkoani Iringa. Utafiti huo ambao umekamilika kwa asilimia 100 umeonyesha uwepo wa jumla ya hekta 11,746 zinazofaa kwa uwekezaji huo, unaotazamiwa kuondoa hali ya uhaba wa sukari nchini.
Malengo ya Serikali ni kuongeza uzalishaji wa sukari nchini na kuiwezesha Tanzania kuwa wauzaji wa sukari kwa nchi washirika wanaoizunguka Tanzania.
Uwekezaji huo pia unatarajiwa kuongeza zaidi ya ajira za moja kwa moja 15,763 na nyingine 21,034 zisizo za moja kwa moja.
Hatua hizi zinalenga kuboresha uchumi wa vijana wa kitanzania kwa kuinua vipato vyao kupitia ajira hizo. Jamii zitakazozunguka viwanda hivi zinatarajiwa kunufaika kupitia miradi ya uendelezaji wa huduma za kijamii itakayokuwa inafadhiliwa na viwanda vitakavyojengwa hapo.
Maelezo hayo yametolewa kwa niaba ya Serikali na Naibu Waziri wa Kilimo Mh. David Silinde alipokuwa akijibu swali la mbunge wa jimbo la Kilolo, Mh. Justin Lazaro Nyamoga, aliyetaka kujua ni lini Seeikali itatafuta mwekezaji kwa ajili ya kilimo cha miwa na kiwanda cha sukari katika kata ya Mahenge Wilayani Kilolo.