Uchambuzi wa Kitaalam: Maandamano yanaibomoa CHADEMA kuliko kuijenga.

Uchambuzi wa Kitaalam: Maandamano yanaibomoa CHADEMA kuliko kuijenga.

Chama cha Demokrasia na Maendeleo ni (CHADEMA), ni chama kikuu cha upinzani nchini Tanzania chenye makao makuu yake jijini Dar es Salaam wilaya ya Kinondoni. Kwa miaka mingi chama hicho kimekuwa kikifanya harakati mbalimbali zenye lengo la kuibua makosa mbalimbali yanayofanywa na chama tawala CCM, harakati hizo wanafanya kwa kuuza sera zao kwa Watanzaia kupita mikutano ya hadhara, maandamano, mitandao ya kijamii, redio na televisheni.

Kwenye sayansi ya siasa tunajifunza ya kwamba chama chochote cha siasa lengo lake kubwa ni kushika dola. Katika nchi za kidemokrasia kama Tanzania, namna pekee inayotumika kushika dola ni kupitia uchaguzi ambapo vyama mbalimbali hushiriki wa watu wanapiga kura kuchagua viongozi kupitia sanduku la kura.

Ili sasa chama cha siasa kiweze kushinda uchaguzi na kushika dola, mtaji mkubwa ni watu. Vyama vya siasa ni kama daraja wanalotumia raia wa nchi husika kufikia malengo yao. Hivyo basi, ili raia waweza kuliamini daraja hilo na walitumie kama njia kuu ya kufikia malengo yao, lazima daraja hilo liwe imara zaidi.

Kwenye hili, tukitazame chama cha CHADEMA kama daraja, na kwa matendo na harakati zake za kila siku, Je, kinajenga imani kwa watanzania kukitumia kama daraja kuyafikia malengo yao?

Moja ya sababu iliyoifanya chama cha CHADEMA kupata wafuasi wengi ni namna inavyoendesha siasa zake. CHADEMA ni chama cha siasa kinachojitahidi kuwa hai wakati wote kufanya harakati kwa kukosoa matendo ya serikali, sheria, miswada, sera na mambo mengine kwa maslahi mapana ya watanzania.

Tangia serikali ya Rais Samia Suluhu iondoe katazo la kutofanya mikutano ya hadhara na maandamano lililowekwa na Serikali ya hayati John Pombe Magufuli, CHADEMA imekuwa mstari wa mbele kwenye kuhakikisha kwamba inatumia vyema nafasi hiyo kujiimarisha kisiasa kwa Watanzania kupitia kufanya mikutano ya hadhara na kufanya maandamano.

Tayari chama cha CHADEMA imeshafanya maandamano katika mikoa mitatu, Dar es Salaam, Mwanza na Mbeya. Katika maandamano hayo CHADEMA inadai mambo makubwa matano yaweze kufanyiwa kazi na serikali. Jambo la kwanza ni kuhakikisha serikali inapunguza ugumu wa maisha kwa kushusha bei ya bidhaa mihimu, pili kuharakisha mchakato wa katiba mpya, tatu kufanya marekebisho ya katiba inayotumika sasa ili kuwa uchaguzi wa haki na huru 2025, nne serikali iondoe miswada mitatu ya vyama vya siasa na uchaguzi bungeni na mwisho serikali lazima iwe ina sikiliza maoni ya wananchi.

Sasa basi, katika maandamano ambayo tayari CHADEMA wameshafanya, yanawajenga au yanawabomoa? Ili sasa tujue kwamba maandamano haya yanawajenga au wanawabomoa, lazima tutazame malengo makubwa ya kufanya maandamano hayo. Bila shaka lengo kuu ni kuona kwamba serikali inafanyia kazi maombi ya CHADEMA kama yalivyowasilishwa.

Bila shaka wananchi watapoteza imani na matumaini kwa CHADEMA kama, watafanya maandamano katika mikoa mbalimbali halafu bado hali ya maisha itabaki kuwa ile ile na kama katika malengo yao, hakutokuwa na lengo hata moja ambalo litafanyiwa kazi na serikali, tija na haja ya maandamano kwa Watanzania itapotea kabisa, pia imani ya watu kwa chama hicho itashuka kabisa kwani, chama hicho hakiwezi kutumika tena kama daraja na Watanzania la kuwavusha kufikia malengo yao.

Tukifanya upembuzi mdogo tu wa maandamano ya Dar es Salaam, Mwanza na Mbeya, ukweli ni kwamba hakuna kitu kilichobadilika na hatua yeyote iliyochukuliwa na serikali inayoonesha kwamba imetokana na shinikizo la maandamano hayo. Ukweli ni kwamba hakuna hata moja. Hali hii sio nzuri kwa CHADEMA na inatoa tafsiri zifuatazo: kwanza, inaonesha maandamano sio suluhu la matatizo ya watu, pili, CHADEMA ni chama dhaifu kwenye kuinishinikiza serikali kutekeleza matakwa yake. Sasa nini kinafuata baada ya hapo? Endelea kusoma.

Imani ya watu kwamba CHADEMA inaweza kuwapa msaada itapotea kabisa, kwani licha ya wao kuacha shughuli zao za kiuchumi na kushiriki maandamano ambayo kimsingi hayajaleta tija yeyote, lakini bado hali ni ileile. Pili, wafuasi wengi wa CHADEMA watahamia vyama vingine vya siasa kutafuta tumaini jipya kwa sababu wamelikosa ndani ya CHADEMA. Kama tulivyosema awali kwamba mtaji wa chama chochote cha siasa ni watu, basi CHADEMA itakuwa kwa kiasi kikubwa imepoteza watu na huo ndio mwanzo wa kupoteza sifa yake kama chama kikuu cha upinzani nchini. Haya sio mageni, yalishaikuta NCCR Mageuzi na CUF.

CHADEMA inavyozidi kufanya maandamano na kuja na matakwa mbalimbali, endapo serikali itaendelea kuyapuuza matakwa hayo kila siku, basi ndio mwazo wa kifo cha CHADEMA kinavyozidi kukaribia kwani, ile kazi ya chama cha siasa kuwa daraja la watu kupita na kufikia malengo yao, itakuwa imepotea na hilo ndio anguko la milele la CHADEMA.

Hii inahitimisha kwamba, katika awamu hii ya Rais Samia Suluhu Hassan ambapo kazi kubwa inafanyika kwenye kuleta maendeleo ya Watanzania, maandamano yana athari mbaya kwa CHADEMA kuliko faida, kwanini? Moja, watu wanaona kazi kubwa inayofanyika, shule zinajenga, miundombinu ya maji ma umeme inaimarishwa, barabara, ajira na mambo mengi kwa maendeleo ya Watanzania hivyo basi, ni ngumu sana kukusanya watu na kuwatembeza barabarani na kuwaaminisha kwamba serikali haiwafanyii kitu watu wake.