Uchumi: Tanzania yaanza kuimarisha hazina ya dhahabu huku baadhi ya nchi za Afrika zikiyumba kiuchumi.

Uchumi: Tanzania yaanza kuimarisha hazina ya dhahabu huku baadhi ya nchi za Afrika zikiyumba kiuchumi.

Historia imeandikwa katika kiuchumi

Historia imeandikwa! Kwa mara ya kwanza baada ya miaka 62 ya uhuru, Tanzania kupitia Benki Kuu ya Tanzania (BOT) imefungua hazina ya kuhifadhi dhahabu ambayo itakuwa inanunuliwa hapa nchini kutoka kwa wachimbaji wa ndani. Sasa Tanzania haitokwenda kutegemea tena hifadhi ya fedha za kigeni pekee iliyokuwa ikiweka kwa miaka yote, bali pia itakuwa na hifadhi ya dhahabu ambayo wachumi wengi na wataalamu wa masuala ya fedha na biashara za kimataifa, wameisifia hatua hiyo na kusema kwamba ni muhimu zaidi kuelekea kuimarisha na kuikomboa Tanzania kiuchumi.

Kinachofanyika

Katika mwaka wa fedha 2023/24, serikali ya Tanzania imepanga kununua tani 6 za dhahabu ambapo hadi hivi sasa kwa mujibu wa Gavana wa Benki Kuu Emmanuel Tutuba, tayari serikali imeshanunua kilo 418 tangu benki hiyo ianze kununua madini hayo Septemba 21, 2023. Hatua hii ya serikali ya Mheshimiwa Rais Samia Suluhu haitokwenda tu kuimarisha uwezo wa serikali kununua kutoka nje, bali pia inakwenda kuimarisha maisha ya watu wa chini kama vile wachimbaji wadogo, ambao nao serikali itawazingatia katika kununua madini kutoka kwao, wachimbaji wa kati pamoja na wakubwa. Wadau wa mbalimbali wa uchumi wanatabiri Tanzania kwenda kufanikiwa zaidi kwenye hili, kwani dhahabu yote ambayo itanunuliwa na BOT, itasafishwa na viwanda vilivyopo ndani, mfano kimoja cha GGR kilichopo mkoani Geita chenye ithibati (Standard) za kimataifa kwenye kusafisha dhahabu.

Hali ilivyo

Tanzania imeanza mchakato wa kuhifadhi dhahabu wakati ambao bado mataifa mengi barani Afrika yanajikwamua kupambana na madhara ya COVID-19 na vita ya Urusi na Ukraine inaendelea barani Ulaya muda huu. Uimara wa uchumi wa Tanzania uliopo sasa haimaanishi kwamba COVID-19 na vita vya Urusi na Ukraine havikuathiri uchumi wake, bali sera bora na usimamizi mzuri wa rasilimali chini ya Rais Samia Suluhu vimechangia kwa kiasi kikubwa kufufua na kuimarisha uchumi kwa haraka zaidi ya ilivyotarajiwa. Mfano, ripoti za kila mwezi za Benki Kuu zinaonesha mfumuko wa bei nchini Tanzania umekuwa ukipungua kwa miezi saba mfululizo, kutoka 4.9% Januari hadi 3.3% mwezi juni. Licha ya dhoruba za kiuchumi duniani, bado Tanzania ilimudu kutoa ruzuku ya zaidi Tsh bilioni 100 kwenye mafuta na zaidi ya Tsh bilioni 150 kwenye mbolea, hali iliyochangia kuimarisha uchumi wa nchi hadi hivi leo.

Hali tete kwa nchi nyingi Afrika

Kama si Tanzania kujiridhisha na hali ya uchumi iliyopo, isingechukua maamuzi ya kuanzisha hifadhi ya dhahabu wakati huu ambao hali ya chumi katika nchi nyingi barani Afrika ni mbaya zaidi. Kwa mfano, taifa la Ghana Septemba 2023 lilitangazwa kufilisika na hivyo kuamua kwenda kulipigia magoti Shirika la Fedha Duniani (IMF) na kuliomba mkopo wa Dola za Kimarekani Bilioni 3 (Tsh trilioni 7) kunusuru uchumi wake. Wakati Tanzania inatumia shilingi kununua dhababu, shilingi ya Kenya imeanguka kwa 17% dhidi ya dola kwa mwaka huu pekee, anguko kubwa zaidi ya fedha hiyo ndani ya kipindi cha miaka 15 iliyopita, ameripoti Mweka Hazina (Treasury Secretary) wa taifa hilo Njuguna Ndung’u.

Takribani nchi zote barani Afrika zimekumbwa na uhaba wa dola, kila nchi kwa namna yake inajaribu kujikomboa kutoka kwenye hali hiyo ambapo Tanzania imeonekana kuchukua hatua madhubuti zaidi ya kununua dhahabu. Uamuzi wa kuwa na hifadhi ya dhahabu utaiwezesha Tanzania kupata fedha za kigeni zitakazowezesha shughuli za kiuchumi lakini pia itakuwa njia mbadala ya Tanzania kutunza dhamana na akiba ya nchini badala ya kutunza fedha taslimu. Faida ya dhahabu inavyozidi kupanda bei kwenye soko la dunia serikali inapata fedha nyingi zaidi tofauti na kutunza pesa taslimu na pia dhahabu ni uwekezaji usiotetereka, ni hifadhi ya uhakika tofauti na dola au fedha nyingine ambapo kuna wakati hushuka thamani.

Hatua ya kununua dhahabu itakwenda kupunguza utoroshaji wa madini hayo kwani wachimbaji wadogo watakuwa wamepata soko la uhakika. Tanzania ni nchini ya nne kwa kuzalisha dhahabu kwa wingi barani Afrika, uwepo wa rasilimali hii nchini unaipa uhakika zaidi Tanzania kuwa hifadhi kubwa ya madini hayo kwenye hazina yake unatoa matumaini ya kwenda kumaliza matatizo yanayosababishwa na upungufu wa dola kama kupanda kwa bei ya mafuta, dawa, mbolea na bidhaa nyingine muhimu.