Rais Samia Suluhu Hassan ameielekeza Ofisi ya Mashtaka kuwafutia makosa vijana wote walioonekana kushiriki maandamano yaliyosababisha vurugu Oktoba 29, mwaka huu, kwa kufuata mkumbo, akisema baadhi yao hawakujua wanachokifanya.
Amelifafanua hilo kwa kile alichoeleza, ukiangalia video za maandamano hayo, kulikuwa na vijana walioingia kuandamana kwa kufuata mkumbo na ushabiki, hawakujua wanalolifanya ndio maana ameomba ofisi ya mashtaka ichuje makosa yao.
Rais Samia ametoa kauli hiyo leo, Ijumaa Novemba 14, 2025 alipozungumza katika hotuba yake ya kulifungua Bunge la 13, jijini Dodoma.
“Nikiwa mama na mlezi wa Taifa hili, ninavielekeza vyombo vya sheria na hasa Mkurugenzi wa Mashtaka kuangalia kiwango cha makosa yaliyofanywa na vijana wetu.
“Kwa wale ambao wanaonekana walifuata mkumbo na hawakudhamiria kufanya uhalifu wawafutie makosa yao,” amesema na kupigiwa makofu na wabunge.
Amesema ukiangalia video za maandamano kulikuwa na vijana walioingia kwa kufuata mkumbo na ushabiki, hawakujua wanalolifanya, ndio maana ameamua kuelekeza wachuje makosa.
“Natoa msamaha huo kwa sababu hata maneno ya Mwenyezi Mungu katika Kitabu cha Luka 23:34 yanasema ‘Yesu akasema Baba uwasamehe kwa kuwa hawajui watendalo” amesema.
