Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi William Shelukindo amesema ziara ya siku tatu ya Rais wa Guinea-Bissau Mh. Umaro Sissoco Embalo inatazamiwa kufungua fursa za kiuchumi kwa watanzania kwa soko la Guinea-Bissau.
Rais Embalo anatarajiwa kuwasili nchini kesho tarehe 21, Juni 2024 ambapo atapokelewa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mh. January Makamba (Mb) Kabla ya mapokezi rasmi kufanyika Ikulu Juni 22, 2024 jijini Dar es salaam.
Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kukutana na mgeni wake Rais Umaro Sissoco Embalo ambae pia ni Mwenyekiti wa Taasisi ya Muungano wa Viongozi wa Afrika katika Kudhibiti Malaria (ALMA), kujadili masuala ya ushirikiano kati ya nchi hizo mbili, yatakayoegemea diplomasia ya uchumi.
Balozi Samwel Shelukindo aliwaeleza waandishi wa habari kuwa, ujio wa Rais Embalo utazalisha fursa za uwekezaji na ushirikiano kibiashara katika matumizi mapana ya Eneo Huru la Biashara Barani Afrika (AfCFTA) ambapo nchi zote mbili zimeridhia uanzishwaji wake.
Wakulima na wafanyabiashara wa korosho kutoka Tanzania wamehimizwa kuwa tayari kuchangamkia fursa zitakazotokana na ushirika baina ya nchi hizi mbili kwani Guinea-Bissau ni moja kati ya nchi zinazozalisha korosha bora duniani.
Katika ziara hiyo, Rais Embolo anatarajiwa kutembelea Miundombinu ya Reli ya Kisasa (SGR) katika Kituo cha Stesheni jijini Dar es salaam. Mbali na hapo Rais huyo wa Guinea-Bissau atatembelea Mamlaka ya Eneo Huru la Uwekezaji kwa Mauzo Nje (EPZA) na pia ataitembelea Taasisi ya Muungano wa Viongozi wa Afrika katika kudhibiti Malaria (ALMA).
Ujio huo wa Rais Embalo ni tafsiri ya mafanikio makubwa ya sera ya Diplomasia ya Uchumi inayotekelezwa na Serikali ya awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.