Utangulizi
Hivi karibuni imeibuka kauli yenye ukakasi kutoka kwa Makamu Mwenyekiti wa Chadema, Tundu Lissu kuwa, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Daktari Samia Suluhu Hassan, ni Mzanzibari ndiyo maana anagawa rasilimali za Tanganyika kwa Waarabu.
Kwanza, si jambo la kubishaniwa kuwa Rais ni Mzanzibari. Ni kweli kwamba Rais wetu anatoka upande wa pili wa Muungano ambao ni Zanzibar. Ila si sahihi kuuhusisha uzanzibari wake na madaraka yake anapotekeleza majukumu yake kama Rais wa Jamhuri ya Muungano.
Madaraka ya Rais hayatokani na wala hayafungwi na upande anaotoka (iwe ni Tanzania Bara au Zanzibar) bali yanatokana na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 na marekebisho yake.
Kwa hiyo, mtu yeyote anayelinganisha madaraka ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na upande anaotoka, ni uthibitisho wa wazi kuwa mtu huyo haifahamu Katiba ya Jamhuri ya Muungano au anafanya hivyo kwa makusudi ili kuupotosha umma kwa lengo la kutimiza maslahi yake binafsi ya kisiasa.
Mfumo wa Muungano
Kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya 1977, mfumo wa Muungano wetu ni wa Serikali mbili. Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Ibara ya 34 (1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano inaeleza kuwa, Kutakuwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano ambayo itakuwa na mamlaka juu ya mambo yote ya Muungano katika Jamhuri ya Muungano, na pia juu ya mambo mengine yote yahusuyo Tanzania Bara. Aidha, ibara ya 34 (3) inaeleza kuwa, Mamlaka yote ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano juu ya mambo yote ya Muungano katika Jamhuri ya Muungano, na pia juu ya mambo mengineyo yote yahusuyo Tanzania Bara, yatakuwa mikononi mwa Rais wa Jamhuri ya Muungano.
Jambo la msingi la kuzingatia katika aya hizo mbili za ibara ya 34 ni kwamba:-
- Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (bila kujali anatokea upande gani wa Muungano) atakuwa na mamlaka kamili juu ya mambo yote ya Muungano katika Jamhuri ya Muungano, na pia juu ya mambo mengineyo yote yahusuyo Tanzania Bara.
- Katika mfumo wa Muungano tulio nao; hakuna kitu kinachoitwa Tanganyika. Kuna Tanzania Bara na Tanzania Zanzibar. Kwa hiyo, kuanza kuibua hoja ya utanganyika ni kujaribu kuuvunja muungano kwa kwa hoja za ubinafsi na ubaguzi .
Wajibu wa Kiongozi/ Mkuu wa Nchi
Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Nyerere aliwahi kusema kuwa “Kazi ya Kiongozi ni kuwaunganisha watu. Kazi ya Kiongozi si kuwagawa watu”
Mtu anayetafuta uongozi kwa misingi ya ubaguzi wa makabila, udini, au ukanda, huyo hafai kuwa kiongozi kwa kuwa anawagawa watu. Kuuzungumzia Uzanzibari na Utanganyika ni ubaguzi wa ukanda (mahali anapotoka mtu). Aidha, ni kuwachochea wananchi kuwa na mtazamo hasi kwa Rais kutokana na sehemu anayotoka. Jambo hilo kamwe haliwezi kuliunganisha Taifa na badala yake mawazo kama hayo hatimaye yatalisambaratisha taifa.
Utaratibu wa Kuingia Mikataba ya Kimataifa
Kwa mujibu wa Ibara ya 63(3)(d) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; ni kazi ya Bunge, kujadili na kuridhia mikataba yote inayohusu Jamhuri ya Muungano na ambayo kwa masharti yake inahitaji kuridhiwa.
Kwa sababu hiyo, ni makosa kufikiri kuwa Rais kwa matashi yake binafsi anaweza kutwaa eneo lolote na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kuwagawia wageni iwe ni kwa shughuli za uwekezaji au shughuli nyinginezo bila Bunge (ambalo ndicho chombo cha uwakilishi wa wananchi) kuridhia.
Athari za Kauli za Tundu Lissu
- Ubaguzi wa ukanda (uzanzibari na utanganyika): kwamba mzanzibari hana haki ya kunufaika na fursa zilizopo upande wa pili wa Muungano hususan fursa ya kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano.
- Ubaguzi wa Uzawa: Kwamba mtu aliyezaliwa eneo fulani hana haki ya kunufaika na fursa zilizopo katika eneo jingine.
- Ubaguzi wa Kikabila: Kwamba kabila fulani halina haki ya kunufaika na fursa zilizopo katika maeneo ya makabila mengine. Kwa mfano, Kwa mujibu wa Sheria za nchi hii; hakuna kabila lenye ardhi yake. Kila kabila la nchi limetapakaa ukanda mwingine mahali ambapo si asili yake ya kuzaliwa. Wamaasai wapo karibu kila mahali hapa nchini, Wachaga vivyo hivyo, Wapo Morogoro, Tanga, Mbeya, Dar es Salaam, Pwani nk. Kama tutatengeneza madai ya ardhi kikabila basi watu wengi wataondoka katika maeneo waliyopo sasa; na hii italeta mtikisiko mkubwa kwenye shughuli za kiuchumi kwa wananchi.
- Kuwavuruga wananchi:- Lissu alipogombea Urais mwaka 2020 aliwaahidi wananchi kuwa ataudumisha muungano kwa kuondoa kero za Muungano, leo anazungumzia Uzanzibari na Utanganyika. Huku ni kukosa msimamo wa kisera na ni kuwavuruga wananchi.
Hitimisho
Kwa mujibu wa Ibara ya 33 (2); Rais ni Mkuu wa Nchi, Kiongozi wa Serikali na Amiri Jeshi Mkuu. Hata hivyo, Rais hutekeleza majukumu yake kwa mujibu wa Katiba, sheria na taratibu zilizopo. Aidha, hutekeleza majukumu yake kwa kuzingatia mipaka ya kiutendaji baina ya mihili mingine ya Dola ambayo ni Bunge na Mahakama.
Kwa kumalizia, ni muhimu kutilia maanani kuwa, Rais kama Mkuu wa Nchi, Kiongozi wa Serikali na Amiri Jeshi Mkuu ni taasisi; na utekelezaji wa majukumu yake unafanyika kitaasisi. Kwa hiyo, ni makossa ku-‘personalize’ majukumu ya Rais na kuyanasibisha majukumu hayo na sehemu anayotoka.
Kufanya hivyo, ni kujaribu kuchafua taswira ya Rais kwa makusudi na kuchochea chuki kwa wananchi dhidi ya Rais jambo ambalo ni hatari kwa amani, utulivu na umoja wa kitaifa. Mtu anayefanya hivyo, kwa vyovyote vile, si mzalendo na kwa sababu hiyo, hafai kuwa kiongozi.
Kauli kama hizi zenye lengo la kumfunga mikono Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kutekeleza majukumu yake, kwa hoja za kibaguzi zinapaswa kupuuzwa na kupingwa na watanzania wote kwa mustakabali mwema wa Muungano wetu na Maendeleo ya Nchi yetu.